Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Alhamisi, 12 Juni 2014

UHAKIKI WA NADHARIA YA KI-MARX KATIKA FASIHI.

Swali.
Eleza mawazo makuu yanayojitokeza katika nadharia ya Umarx kisha hakiki Tamthilia ya Kwenye Ukingo wa Thim kwa kutumia nadharia ya Ki-Marx.
DONDOO:
UTANGULIZI
  Maana ya Nadhari
  Maana ya Umarx
  Maana ya Nadharia ya Umarx
  KIINI
  Mawazo makuu yanayojitokeza katika nadharia ya Umarx.
 Sifa na udhaifu wa nadharia ya Ki-Marx
 Uhakiki wa Tamthilia ya Kwenye Ukingo wa Thim.
·        HITIMISHO
·        MAREJEO
Nadharia ni dhana iliyofafanuliwa na wataalam mbalimbali kama ifuatavyo:
Wafula na Njogu,(2007:7) Nadharia ni jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.
Tuki, (2004:300) Nadharia ni mawazo, maelezo au muongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani.
Tunakubaliana na fasili iliyotolewa na Wafula na Njogu, kutokana na kwamba fasili hii imetaja vitu muhimu kama vile, maelekezo ambayo ndiyo yanayomuongoza msomaji au mhakiki ili asivuke mipaka ya mawazo ya hiyo nadharia aitumiayo ili kufanikisha kazi kwa ufasaha.
Maana ya Umarx:
Wamitila,(2006:182) anasema, umarx ni falsafa ya kiyakinifu hasa kwa kuwa pana msisitizo mkubwa kwenye msingi wa hali za kiyakinifu za maisha kama mazingira ya kuishi kuliko mawazo katika maisha ya binadamu (ikimaanisha kwamba mawazo yake hayategemezi kwenye dhana dhahania kama urembo, ukweli au ndoto bali anayategemeza kwenye uhalisia unaoonekana.
Nadharia ya umarx ilianzishwa na Karl Marx mwaka 1818-1863 na Fredrich Engles (1820-1895).Katika nadharia hii Marx amejikita katika historia na miundo ya kijamii kwa kupitia hoja kuu zifuatazo.
Historia ya maisha ya binadamu inaweza kuelezeka katika misingi yakinifu ya kiuchumi ambayo itachunguza njia za uzalishaji mali pamoja na miundo ya kiuchumi na pia huathiri uzalishaji mali na usambazaji wa mali hizo. Hivi vyote kwa pamoja huunda misingi ambapo kwenye misingi hiyo huunda maadili, itikadi, dini na utamaduni.
Hoja nyingine ni kuamini kuwa historia ya binadamu inadhihirisha au kuakisi harakati zinazoendelea katika matabaka ya kiuchumi-jamii. Marx alisema “Historia ya maisha ya binadamu ni ya harakati za kitabaka”.
Harakati za kitabaka katika jamii. Nadharia ya ki-marx inaangalia matabaka katika ngazi mbalimbali kama vile ngazi ya familia, dini na elimu.
Ubepari kama njia ya uzalishaji mali na mara nyingi huharibiwa na tabaka la chini, hivyo ubepari hujitengenezea njia za kujiharibu wenyewe. Kutokana na unyonyaji na ukandamizaji unaoufanya kwa tabaka la chini.    
Njia ya kuondokana na ubepari huu jamii  lazima ikemee.
Mshikamano uliopo baina ya tabaka tawaliwa. Kwa mujibu wa marx ili kuondokana na mfumo wa unyonyaji na ukandamizaji, jamii lazima iungane ili kubadilisha mfumo uliopo.
Matamanio ya kitabaka yanaakisi jamii hiyo au itikadi ya jamii iliyopo. Kwa mujibu wa nadharia ya umarx tabaka la chini itikadi yao ni kupambana na tabaka la juu ili kuondokana na unyonyaji na ukandamizaji na tabaka la juu itikadi yao inaonekana kuwa ni halali kulikandamiza tabaka la chini.
Fasihi inayojitokeza inaweza kuyaakisi au kuyadhihirisha mahusiano ya nguvu katika jamii, matamanio na matakwa ya matabaka yaliyopo katika jamii yanaakisiwa katika itikadi iliyopo katika jamii.
Sifa za Uhakiki wa kimarx:
Kuna muelekeo mkubwa wa kuitazama sanaa katika nadharia hii kwa kutilia mkazo mkubwa kwenye dhamira.
Ni mkabala ambao unaingalia fasihi kwa kuhusisha na mazingira yake ya kihisitoria pamoja na shughuli zingine za kibinadamu.
Ni nadharia inayopinga au mtazamo wa kubagua au kutenga fasihi na mazingira yanayoizaa kama ilivyooneshwa kwenye nadharia nyingine kadhaa.
Kwa kuhimiza kuchunguzwa vipengele vya kijamii na kiuchumi uhakiki unaelekea kupanua uwanda wa fasihi.
Udhaifu wa nadharia hii ya Kimarx:
Uhakiki wa Ki-marx unaishia kuidunisha na kuipuuza kazi ambayo ina sifa za kiwango cha juu sana za kiujumi au kisanaa kwa kuwa ni dhaifu kiitikadi  licha ya kuwa itikadi sio kaida au kanuni ya sanaa au ubunifu. Hatuwezi kupuza kazi kwa misingi ya kiitikadi tu.
Hivyo huzichunguza sifa mbalimbali za kazi ya kifasihi pale tu zinapoingiliana na miundo ya kihistoria jamii au kiuchumi kwa kufungamana na itikadi yake.
Matokeo ya mtazamo huu wa kuyamulika zaidi masuala ya kidhamira yanaifanya nadharia hii kutoangaza vipengele vingine vidogovidogo ili kutathimini ubunifu au upekee wa kazi inayohusika.
Unaelekea kuchunguza muktadha wa kihisitoria kwa kuelemea mno kwenye vigezo vya kiuchumi.
Jamii ni kielelezo kinachoshikiliwa kama upeo wa kuendelea na kusambaratika kwa mfumo wa kibepari unaoelekea kuwa na elementi za kinjozi.
Namna ya kutumia uhakiki wa Ki-marx katika kazi za kifasihi.
Miaka ya hivi karibuni uhakiki wa kazi za kifasihi umezidi kupanuka katika kuelezea masuala ya kijamii na kisiasa. Hivyo unapotumia uhakiki wa ki-marx katika kazi za kifasihi lengo ni kuonesha tofauti za kijamii, kisiasa, kiuchumi kulingana na maelezo yalivyo katika kitabu. Hii inaonesha itikadi ya kijamii ya mwandishi na kuweka uhusiano kati ya uzoefu wa kijamii wa mwandishi na wa wahusika wake.
Katika kutekeleza itikadi za uhakiki wa ki-marx kuna hatua tano za kufuata ili kuhakiki kazi ya fasihi kwa ufanisi.
Kueleza jinsi wahusika wanavyohusiana:                                                                          Uhusiano baina ya watu, muingiliano wao utaonesha madaraja na ishara fulani zinazoendana na tofauti za matabaka ya kijamii.
Kutathimini kazi za wahusika:                                                                           
Uhusika wao umejikita katika mifumo ya kimatabaka ambapo kazi anayofanya mhusika inaashiria moja kwa moja sehemu alipo katika mfumo. Kiwango cha anasa na kiwango cha utendaji kazi navyo vinaonesha sehemu alipo katika mfumo.                                                      
Kuonesha jinsi wahusika wanavyotumia muda wao wa mapumziko.                   Nadharia ya ki-marx inaeleza kuwa mtu anauwezo wa kutumia muda wake wa mapumziko kwa namna ya uzalishaji mali au anavyopenda yeye. Huu muda wa kupumziko huashiria namna mtu anavyoishi na jamii inayomzunguka.
Kutathimini jukumu la serikali, 
kuonesha mfumo wake, vyombo vya utekelezaji na jinsi jamii inavyopokea mafanikio yake.                                                                                                 
Kurejea waandishi wengine wa ki-marx na kutafiti vipindi ambavyo kazi hiyo ya kifasihi imechapwa na kisha kuhusianisha mawazo yaliyotolewa na kipindi hicho.
Kulingana na mawazo ya ki-marx yaliyofafanuliwa hapo juu tunaweza kuhakiki tamthiliya ya “Kwenye Ukingo wa Thim” kama ifuatavyo:
Tamthiliya ya Kwenye Ukingo wa Thim iliyoandikwa na Ebrahim Hussein (1988). Hussein ni mtunzi maarufu sana ambaye ameumudu usanii wa tamthiliya za Kiswahili. Miongoni mwa Tamthiliya zake ni Kinjeketile, Mashatani, Arusi na Kwenye Ukingo wa Thim. “Kwenye Ukingo wa Thim” inaonesha migogoro iliyopo ya kitabaka baina ya mahitaji ya mila na maisha ya kisasa, utawala na utawaliwa, vilevile kuna utabaka wa kipato cha juu na cha chini, utabaka wa kielimu (waliosoma na wasiosoma). Vilevile ameonesha harakati za kuondoa matabaka hayo.
Uhakiki wa kitabu utafanyika kwa kujikita zaidi katika nadharia ya ki-marx.
Tukianza na kipengele cha maudhui dhamira zilizojitokaza ni kama ifuatavyo:
Dhuluma na unyonyaji: Mwandishi amemtumia Martha kuonesha dhamira hii. Ameonesha jinsi Umma klani ulivyomnyang’anya Martha mali zake zote baada ya kufiwa na mumewe.
Mfano; ukurasa.33 “mawe yanavunja viyoo kikundi cha watu kimeingia.Wanaimba mchaka mchaka chinja…wanachukua vitu, mapambo, glasi wanaondoka….”
Suala la dhuluma lipo katika jamii hiyo, basi kutokana na nadharia ya umarx anaonesha kuwa ili jamii iondokane na dhuluma lazima ipambane ili kuliondoa tabaka la unyonyaji.
Matabaka: mwandishi ameonesha suala hili jinsi linavyojidihirisha wazi kati ya wenyenacho na wasionacho. Mfano; familia ya Herbert, hawa ndiyo wenyenacho na wasionacho ni kama vile Stella (ukurasa.1), watawala na watawaliwa , mfano; viongozi kama DC, na watawaliwa mfanyakazi wa kwanza na mfanyakazi wa pili (19-20), wasomi na wasiosoma. Wasomi kama vile Herbert, Chris, Jean na Ben. Na ambao si wasomi ni kama vile Stella, George na Mzee. Suala hili la matabaka katika jamii ni suala la kiyakinifu ambalo limejidhihirisha dhahiri katika jamii. Hivyo kwa mtazamo wa ki-marx unatoa pendekezo kuwa ili jamii ijikomboe na matabaka lazima ifanye mapinduzi.
Ubepari: mwandishi ametumia mawazo ya mfumo wa uzalishaji mali wa kibepari kwa kuonesha tabia za mfumo huo kwa mfano; watu kumiliki majumba makubwa, magari, viwanja, makampuni nk. Mfano;
Veranda kubwa ina vitu vizuri. Vitu vyenye thamani, ina mapambo, vitu vya shaba…”(ukurasa.1)“Kazi nyingi viwanja bado havijalipiwa kodi mwaka huu,halafu Stella hana mahali pa kukaa toka zile nyumba walizokuwa wakikaa kubomolewa na kujengwa afisi mpya za kampuni mpya ya Kiamerika (ukurasa.5)”
Suala la ubepari katika jamii linajidhihirisha dhahiri, kwani kuna watu wanamiliki mali nyingi bila usawa wakati wengine hawana kabisa. Hivyo Marx anatoa pendekezo kuwa ili jamii iwe na usawa lazima kuwe na umiliki sawa wa mali katika jamii.
Uongozi mbaya: mwandishi ameonesha uongozi kama tabaka ambalo linafanya kazi kwa maslahi ya tabaka hilo. Hali hii inajidhihirisha katika sehemu za mjini ambako hukaa viongozi au watawala, huko ndiko kuna maendeleo ya kijamii na kiuchumi ambapo watu wenye kipato cha juu huishi, lakini tabaka tawaliwa ambalo wengi wao wanaishi kijijini limeoneshwa kutopewa huduma muhimu za kijamii. Mfano, miundombinu mibovu kama vile barabara na hata maji hakuna. Utaona kwamba juhudi za kujenga barabara pamoja na kisima cha maji kule kijijini ilikuwa ni kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya Herbert kwa vile ni kiongozi lakini haikuwa nia ya kuleta maendeleo katika kijiji hicho. Mfano katika (ukurasa.19)
Mfanyakazi I: “Tumekuja kutengeneza barabara.Wapi ile daraja mbovu. Tunataka kutengenesa haraka sana”.
Mfanyakazi wa II: “Na kisima? Kisima cha kijiji kiko wapi?Tunataka tasama kama maji safi”.
Hapa katika nadharia ya umarx inasema kwamba ili jamii iondokane na uongozi mbaya unaojali tabaka tawala lazima tabaka tawaliwa lipambane ili kuondokana na uongozi mbaya katika jamii.
Dini: suala hili limeweza kijitokaza pale Herbert alipokufa, mkewe (Martha) aliponyang’anywa mali zote na Umma Klan. Tunaona kwamba Martha aliamua kupambana ili aweze kukomboa mali zake lakini Pasta alimkataza na kumuambia amuachie Mungu.
Mfano katika (ukurasa.32) Pasta:“M-a-a-r-th-a-a! Martha! Mlani shetani. Martha!”
 Martha: (Anarejesha bunduki. Pasta anaichukuwa. Anairejesha mahali pake)                                               
Kwa mujibu wa nadharia ya Umarx inasema kwamba, dini ni kama kilevi cha kuwalewesha au kuwapumbaza watu na kuwafumba fikra zao wasiendelee na harakati za kujikomboa.
Ujasiri: mwandishi ameonesha dhamira ya ujasiri kwa kumtumia Martha, dhamira hii imejidhihirisha pale ambapo shemeji yake (George) alipochukua hati ya nyumba yake. Martha alichukua bunduki na risasi na kutaka kumlenga George. Hivyo Martha aliweza kuonesha ujasiri katika kukomboa mali zake. 
Hii inajitokeza katika (ukurasa.32)
“…Martha anachukua bunduki. Anachukua risasi kwenye mtoto wa meza. AnamlengGeorge”.
Kwa mujibu wa nadharia ya Umarx katika suala la kupinga unyonyaji unahitajika ujasiri na mapambano ili kuhakikisha usawa unapatikana kwa wote, na kusiwepo na unyonyaji wala ukandamizaji.
Umoja na mshikamano: suala hili limejitokeza pale ambapo jamii ilivyoweza kupigana na kuweza kurudisha tena ardhi yao mikononi mwao. Hii inaonesha hapo awali walikuwa na ushirikiano mpaka wakaweza kurudisha ardhi yao. Na vilevile wanaitukuza kwa mila zao.
Katika (ukurasa.23) Mzee: “….Ardhi hii ni yetu.Mali yetu. Toka enzi za Ruoth. Mkuki na bunduki iliteka ardhi hii. Ni yetu. Tumeilipia kwa damu. Na tunaitukuza kwa mila zetu…”                 
Pia umoja na mshikamano umejitokeza kwa kupitia akaunti ya pamoja ya kijiji, ambapo mapato yote ya kijiji yana milikiwa na kijiji. Mfano (ukurasa.19) Muuza duka:  “nataka pesa za ndoo mbili, ufagio, chumvi; mbao”. 
Mzee:“Andika katika akaunti ya kijiji”.                                                                                                                                                                                
Nadharia ya Umarx inasema kwamba, kama jamii ikiwa na umoja na mshikamano basi matabaka ya aina yoyote hayatakuwepo na umilikaji mali utakuwa ni wa jamii nzima katika hali ya usawa.
Kutokana na nadharia ya umarx tunaweza kuchambua baadhi ya vipengele vya maudhui;
Migogoro: migogoro iliyoonekana katika tamthilia ya Kwenye Ukingo wa Thim ni pamoja na mgogoro kati ya serikali na wananchi  wa kijijini pale ambapo wanakijiji walikuwa wanapinga serikali juu ya utengenezaji wa barabara na kisima kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya Herbert. Mfano, (ukurasa.19) Mzee:  “Barabara tunatengeneza sisi wenyewe. Ni kazi ya kijiji. Ni wajibu wetu. Wajibu wa Umma Klan”.
Vilevile kulikuwa na mgogoro kati ya Martha na Umma Klan pale ambapo Martha alinyang’anywa mali alizoachiwa na mume wake baada ya kufariki.
Kwa mujibu wa Marx migogoro hainabudi kuwepo katika jamii. Na ni lazima pawepo migogoro ndani ya jamii yoyote ya kitabaka ili kuleta maendeleo.
Falsafa: (Ni mwelekeo wa imani ya msanii juu ya kazi aliyoiandika au ni mawazo makuu ya mwandishi kuhusu maisha). Falsafa ya mwandishi ni ya kimapinduzi, yaani anaamini kuwa ili kuweza kuleta maendeleo au kuleta mabadiliko katika jamii ni lazima kuwepo na mapinduzi dhidi ya matabaka, unyonyaji, ukandamizaji na unyanyasaji. ndipo kutakuwa na usawa katika jamii. Hivyo basi moja kwa moja falsafa hii ya mwandishi inaendana na falsafa ya Ki-marx ambayo ni ya kimapinduzi.
Msimamo: (Ni itikadi anayoishikilia mwandishi ambapo hawezi kuyumbishwa juu ya mtazamo wake). Mtazamo wa mwandishi wa tamthilia hii ni wa kiyakinifu, kwani ameonesha mapambano ya kimatabaka ambayo yanaweza kuhalisika katika jamii. Vilelvile uhalisia huu unajidhihirisha katika nadharia ya Umarx.                                                    
Pia nadharia ya umarx inaweza kutumika katika kuchambua baadhi ya vipengele vya fani ambavyo ni;
Wahusika: mwandishi amewaumba wahusika kwa namna inayosadifu matabaka yao. Mfano;Herbert anawakilisha tabaka la juu, kwani ameonekana kumnyonya mafanyakazi wake wa ndani ambaye ni Stella. Katika (ukurasa.2) Stella muda wote alionekana akifanya kazi bila kupumzika.
Vilevile Stella amechorwa kama mwakilishi wa tabaka la wanyonywaji, kama anavyoonekana akitumikishwa sana, na hata hakuwa na mahali pa kuishi baada ya nyumba alimokuwa anaishi kubomolewa ili kupisha ujenzi wa kampuni mpya ya kiamerika. Rejea ukurasa.5 Hebert; “…Halafu Stella hana mahali pa kukaa…”                                                                 
Martha naye amechorwa kama mnyonywaji hasa pale aliponyang’anywa mali zote na ndugu wa mume wake hali iliyopelekea kifo chake.
Mandhari: mwandishi ametumia mandhari mbalimbali kama vile mandhari ya mjini kuwakilisha eneo linalokaliwa na watu wa tabaka la juu, wasomi na tabaka tawala. Mfano familia ya Herbert mali walizokuwa nazo kama majumba, magari, inaonekana katika ukurasa.2
Mwandishi pia ametumia mandhari ya kijijini kuwakilisha tabaka tawaliwa, watu wa kipato cha chini na wenye hali duni ya maisha. Mfano; Mzee, mfanyakazi wa kwanza na wapili pamoja na Lydia.
Matumizi ya Lugha: kwa kiasi kikubwa lugha iliyotumika ni ya kitabaka yaani lugha inayotumiwa na wasomi au watu wa tabaka la juu ni tofauti na lugha inayotumiwa na watu wa tabaka la chini. Mfano, (ukurasa. 20)
D.C:   “Nani ametoa amri ya kutengeneza barabara?” (utawala) Mfanyakazi 1:   “Ni serikali sir” D.C:   “Rudisha trekta na vyombo vyote vya kazi” P.S:   “kwa nini daraja haitengenezwi? Kwa nini darajambovu?” D.C:   “Haya anza mara moja. Tengeneza barabara.” Mfanyakazi 1 “Yes sir”.
Hivyo inaonesha wazi kwamba lugha anayoitumia D.C na P.S ni ya kiutawala huku Mfanyakazi 1 akitumia lugha ya unyenyekevu.
 Kwa kuhitimisha, nadharia ya umarx ni nadharia inayosawiri masuala ya kiuchumi-jamii kiyakinifu. Hata hivyo ina sifa na udhaifu wake kama ilivyooneshwa hapo awali.
Kuhakiki kwa kutumia nadharia hii kumejikita sana katika kipengele cha maudhui na kugusa kidogo sana au kupuuza kabisa vipengele vya fani ambavyo navyo ni muhimu sana katika kazi za fasihi. Hivyo basi katika uhakiki wa kazi za fasihi nadharia moja haijitoshelezi kuhakiki kitabu.  Hivyo ili mhakiki wa kazi za kifasihi aweze kufaulu vizuri ni lazima atumie nadharia zaidi ya moja katika kuhakiki vipengele vya fani na maudhui, kwani nadharia moja haijitoshelezi kuhakiki vipengele vyote.                             
MAREJEO:
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.Oxford University Press East Africa Ltd. Nairobi.
Hussein, E.(1988). Kwenye Ukingo wa Thim. Oxford University Press East Africa Ltd. Nairobi.
Wamitila, K.W (2002). Uhakiki wa fasihi, Misingi na vipengele vyake. Phoenix Publishers Ltd. Mombasa.
Wafula, R. M na Njogu, K (2007). Nadharia za uhakiki wa Fasihi. Sai Industries Ltd. Nairobi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni